Tuesday , 26th Aug , 2014

Mabondia chipukizi na vijana wadogo wenye vipaji na uwezo katika mchezo wa masumbwi huku wakionesha nidhamu ya hali ya juu ndio watapewa nafasi ya kuunda kikosi kipya cha timu ya taifa ya ngumi za ridhaa ya Tanzania kupitia michuano ya ngumi taifa

Wachezaji wa timu ya ngumi za kulipwa ya Tanzania wakiwa katika moja ya safari ya kwenda nje ya nchi.

Shirikisho la ngumi za ridhaa nchini Tanzania BFT linawaomba wadau wa michezo na makampuni kusaidia ama kudhamini mashindano ya taifa ya ngumi ambayo yanataraji kufanyika mwezi ujao jijini Dar es salaam ili kuyafanya yawe na tija na ubora ambao utasaidia kupata mabondia wenye uwezo na kuunda kikosi imara cha taifa

Katibu mkuu wa BFT Makore Mashaga amesema kuwepo kwa udhamini wa mashindano hayo yatasaidia kuleta tija na hivyo BFT kutimiza lengo la kupata kikosi kipya na bora cha timu ya taifa ya ngumi ambacho baadae kitaandaliwa kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo michuano ya Afrika, dunia na hata michuano ya Olimpiki ya mwaka 2016

Aidha Mashaga amesema uamuzi wa kuunda kikosi kipya cha timu hiyo tena chenye damu changa za mabondia vijana wenye vipaji ni kutokana na kikosi cha timu ya sasa kutofanya vema katika michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ya jumuiya ya madola ambayo ilifanyika hivi karibuni huko jijini Grascow Scotland na Tanzania kuambulia patupu kitu ambacho kimewafanya BFT kuchukua hatua za haraka ili kuondokana na hali hiyo.