Friday , 28th Aug , 2015

Beki na kiungo mkabaji wa Simba, Abdi Banda ameondolewa katika kikosi cha Taifa Stars kitakachoivaa Nigeria katika mechi itakayopigwa jijini Dar es Salaam Septemba 9 mwaka huu kutokana na kuwa majeruhi.

Katika taarifa yake, Kocha wa Stars Charles Boniface mkwasa amesema, Banda hataweza kuivaa Nigeria na sasa mazoezini ameshaondolewa kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja yaliyotokana na mazoezi ya kukimbia kwa kasi ndani ya mita 100.

Kuhusiana na hilo, Daktari wa Taifa Stars, Michael Yomba amesema Banda ameumia nyama ambazo ni lazima kupumzika na kihesabu mapumziko hutakiwa kuanzia siku kumi hadi 21 hivyo anatakiwa kupumzika siku 21 hata baada ya kurejea Simba.