Wednesday , 19th Aug , 2015

Timu ya Azam FC imesema inaendelea na maandalizi isipokuwa itamkosa Kipre Michael Balou kutokana na kuwa majeruhi pamoja na Allan Wanga ambaye bado yupo kwao kwa ajili ya kuhudhuria mazishi ya mama yake yanayotarajiwa kufanyika Agosti 22.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa Habari wa Timu ya Azam FC Jafari Iddy Maganga amesema, timu imewasili jana ikitokea visiwani Zanzibar ambapo iliweka kambi ya siku 13 na kucheza mechi tatu za kirafiki na kushinda zote huku wakiwa na mechi 13 za maandalizi ya ligi kuu ambazo zote pia wameshinda bila kuruhusu goli hata moja.

Azam FC inashuka dimbani uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Agosti 22 mwaka huu dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ni ufunguzi wa pazia la ligi kuu ya Soka Tanzania Bara.

Kwa upande wa usajili, ambapo dirisha lake linatarajiwa kufungwa hapo kesho, Maganga amesema wameshamaliza usajili kwa nafasi zote ambazo kocha alikuwa anaona zina mapungufu na wanaamini usajili huo utaisaidia timu kufikia malengo.