Wednesday , 13th Jul , 2016

NAIBU Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura, amesema kuwa serikali itaajiri Maafisa habari mkoa, michezo, sanaa na utamaduni ili kutatua changamoto mbalimbali za wasanii na wanamichezo katika ngazi za halmashauri hadi Mkoa.

NAIBU Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura.

Aidha amesema kuwa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA) kinamapungufu mbalimbali na kuahidi kushughulikia suala hilo ili viongozi wa chama hicho waheshimiane ikiwemo uongezeko la vipaji.

Wambura amesema hayo leo Jijini hapa wakati alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama vya michezo aliokutana nao ukumbi ulipo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda.

Amesema ameona changamoto mbalimbali zinazowakabili wasanii pamoja na wanamichezo wa aina mbalimbali lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa viwanja na wizi wa kazi za wasanii.

Wambura amesema endapo Maafisa habari hao na Maafisa michezo wakiajiriwa ngazi ya halmashauri wataweza kuhakikisha michezo inakuwa na vipaji vya watoto vinaibuliwa ili kuleta maendeleo kwa Taifa.

Pia amekemea matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwenye michezo pamoja na unywaji wa pombe lakini pia amesisitiza utiii wa sheria ili kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani.

Wakitoa malalamiko yao kwa Naibu Waziri Wambura baadhi ya wadau hao akiwemo Dina Patrick amesema wao wanashule maalum kwaajili ya michezo kwani wao wanakituo maalum cha michezo kinachojulikana kwa jina la St, Patrick Sport Academy lakini wanahitaji kuongeza eneo kwaajili ya kujenga hoteli yenye hadhi ya nyota tano pamoja na kuongeza michezo mbalimbali ikiwemo uwezo wa kuchukua watu 20,000.

Naye Juma Kittley amemwomba Naibu Waziri kusaidia ili mpira wa Rugby uweze kutambuliwa kwenye shule mbalimbali za Mkoa wa Arusha huku Meneja wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Jackson Njoorwa akiiomba serikali kuwasaidia kupata mfadhili kwaajili ya kuukarabati Uwanja huo pamoja na uwekaji wa nyasi bandia.