Thursday , 7th Feb , 2019

Bodi ya ligi nchini (TPLB), imesema malalamiko ya vilabu juu ya ratiba ya ligi hayakwepeki lakini yanatakiwa kupelekwa kwenye Bodi moja kwa moja na sio klabu kulalamika kwenye vyombo vya habari.

Boniface Wambura

Akiongea leo na www.eatv.tv, Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura amesema wao kama Bodi sio kwamba wanajisikia tu kubadilisha ratiba lakini ukweli ni kwamba changamoto mbalimbali ikiwemo viwanja ndio inapelekea kupanguliwa kwa ratiba.

''Watu wanatakiwa kujua kuwa ukibadilisha mechi moja kuna uwezekano mkubwa ikaathiri mechi zingine kutokana na miundombinu yetu na haiwezekani klabu zote zikaridhika na ratiba moja kwa moja ndio maana kunakuwa na malalamiko japo hayatufikii'', amesema.

Aidha Wambura amesisitiza kuwa klabu inapoona ratiba si rafiki au kuna changamoto inatakiwa kuwasilisha maombi kwa bodi ya ligi lakini wengi wao wanalalamika kwenye vyombo vya habari na wanashindwa wajibu nini wakati wanajua bodi ni ya ligi na inaundwa na vilabu vyenyewe na ina ofisi zake pia.

Hivi karibuni meneja wa Yanga Hafidh Saleh na kocha Mwinyi Zahera walinukuliwa wakilalamikia ratiba ya mechi zao mbili dhidi ya Singida United na JKT Tanzania ambapo timu hiyo imelazimika kusafiri zaidi ya kilometa 30 ili kuweza kucheza mechi hizo ndani ya wiki moja.