
Akizungumzia suala hilo kupitia 'Mtu Kati' ya DADAZ inayorushwa na tinga namba moja kwa vijana EATV kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa, Farida Hassan ambaye ni mchumi na mjasiriamali amesema kuwa wanaume wengi wanapokosa pesa hukosa pia kujiamini katika maamuzi.
Farida ameongeza kuwa wanaume wengi wanajua kutafuta pesa lakini sio kutunza pesa tofauti na wanawake, hali ambayo hupelekea migogoro muda mwingine endapo mke asipokuwa na uwezo wa kumsaidia mumewe katika kupangilia matumizi.
"Mipango na masharti yanatakiwa kuwekwa katika matumizi ya pesa hii ni kutokana na asili ya wanaume ni watafutaji lakini sio watunzaji, wanaume watunzaji ni wachache sana", amesema Farida.
Akizungumzia suala la mume kumkopesha mke pesa kwa ajili ya kufungua biashara amesema kuwa linawezekana nasi kitu cha ajabu endapo kila kitu kikifanywa kwa mipango ya maendeleo wala sio uchoyo kama wengi wanavyodai, kwani wanawake wengi wamejiwekea utamaduni wa kupewa kila kitu hali ambayo sio sahihi.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika nchi za Denmark na Marekani umebaini kuwa wanaume wanaopata mshahara mdogo, hawashiriki tendo la ndoa kwa ufanisi na wake zao walio na mishahara mikubwa, ukilinganisha na wanaume walio na kipato kikubwa kuwazidi wake zao.
Msaidizi katika utafiti huo Dkt. Lamar Pierce ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Mipango katika Chuo Kikuu cha Washington alisema kuwa wanaume huwa dhaifu kiutendaji katika tendo la ndoa, inapotokea mwanamke ana cheo au kipato kikubwa kuliko yeye.
Mtafiti huyo alisema kuwa hali hiyo ni mbaya zaidi katika nchi za Afrika, ambapo mfumo dume umetawala huku mapinduzi ya kijinsia yakianza kushika kasi.