Mhandisi Stella Manyanya akiwa Kikaangoni
Ametoa kauli hiyo katika ofis za EATV wakati akijibu maswali ya wananchi kupitia kipindi cha KIKAANGONI kinachoruka kila Jumatano kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV.
Alilazimika kutoa kauli hiyo kutokana na malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kampala tawi la dar es Salaam walioandamana hadi ofisi za wizara hiyo wakilalamika kukosa mikopo kwa madai kuwa mikopo hiyo inatoka kwa ubaguzi wa kivyuo.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa wanafunzi hao wanapaswa kufuata taratibu za kufahamu ni jinsi gani mikopo hiyo inavyotolewa na wafuate utaratibu wa kutoa malalamiko na serikali itaweza kuyachukulia kama changamoto na kuyatatua.
Kuhusu madai ya wanafunzi hao, Manyanya amesema amewasikiliza na kubaini kuwa kuna baadhi yao wana hoja za msingi ikiwemo kuwa na vigezo kama vile uyatima na kozi za vipaumbele, lakini akawataka watafute viambatanisho vya ushahidi wa vigezo vyao, na kisha wafuate taratibu za kukata rufaa kupitia Bodi ya Mikopo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Manyanya amewataka viongozi wa vyuo mbalimbali wasikilize kero za wanafunzi wanaowaongoza na kuzipeleka sehemu husika na siyo kufanya mgomo na maandamano jambo ambalo haliwezi kusaidia katika utatuzi wa kero zao.