Dkt. Vincent Mashinji - Katibu Mkuu CHADEMA
Dkt. Mashinji alitoa kauli hiyo hivi karibuni kupitia kipindi cha KIKAANGONI kinachurushwa kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV, ambapo mwananchi mmoja alitaka kujua mtazamo wake kuhusu dhana ya siasa kuwa mchezo mchafu na ni kwanini yeye aliamua kuingia kwenye siasa wakati akijua kuwa ni mchezo mchafu.
"Siasa siyo mchezo mchafu, hata kwa Mungu kuna siasa na ndiyo maana kulikuwa na utawala, hata yeye anapenda siasa ndiyo maana ameileta, siasa ni mfumo wa maisha, na ndiyo maana hakuna jambo lolote la maendeleo litaweza kufanyika bila siasa, siasa ni mfumo wa uongozi, siyo kweli kuwa siasa ni mchezo mchafu" Alijibu Dkt. Mashinji.
Aidha Mashinji ambaye ni daktari wa binadamu, amesema aliingia kwenye siasa miaka mingi iliyopita, na kwamba siyo mgeni kama ambavyo watu wengi wanadhania na kuongeza kuwa awali alikuwa ni mwanachama wa CCM lakini alipoona anaweza kuwa kiongozi na kusaidia maendeleo alijiunga na CHADEMA kwa kuamini kuwa ni chama kinachoweza kuliletea taifa maendeleo.
"Nimewahi kuwa mwanachama wa CCM, lakini ni katika kipindi ambacho ilikuwa ni lazima uwe na kadi ya CCM ili upate huduma au fursa fulani, kwahiyo nilikuwa na kadi lakini sikuwa na mapenzi na CCM" Alisema Dkt Mashinji na kuweka wazi kuwa yeye bado ni mwanataaluma katika fani ya udaktari na pia ni mtendaji wa chama ambaye hahitaji kuwa mtu wa majukwaani bali mtu anayefanya kazi kimyakimya.