Tuesday , 10th Nov , 2015

Msanii kutoka kundi la Wagosi wa Kaya Dkt. John, amethibitisha kufa kwa kundi hilo na kuanzisha kundi jipya la muziki kutoka mkoani Tanga linaloitwa The Family.

Dkt. John ameyasema hayo kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kueleza kuwa lengo la kuanzisha kundi hilo ni kuufanya mkoa huo usikike tena kwenye Tasnia ya muziki.

"Ni kwamba mimi kama Dkt John kutoka kundi la Wagosi wa Kaya nimeamua sasa hivi kuanzisha familia yangu, kwa malengo mazuri tu ya kufanya Tanga sasa hivi isikike katika muziki huu wa Hip Hop", alisema Dkt John.

Dkt. John ameendelea kusema kwamba sasa hivi muziki umekuwa ni biashara nzuri, hivyo lazima uheshimiwe kwani kuna watu wengi wanaishi kupitia muziki huo.

"Muziki sio tena lele mama kama zamani unatania tania, muziki ni biashara kwa sababu Dj anaishi kwa sababu ya muziki, mwanamuziki anaishi kwa sababu ya muziki ana familia, promota anaishi kwa sababu ya muziki, hivyo muziki inabidi tuuheshimu", alisema Dkt John.

Dkt. John ameendelea kwa kusema kwamba kuhusu kundi lake la wagosi wa Kaya hakuna kitu chochote kinachoendelea, na iwapo kungekuwa na lolote kungekuwa na taarifa.

"Na swala la kuhusu harakati za albamu ya Wagosi wa Kaya, watu wangesoma kwenye mitandao au wangesoma kwenye magezeti au radio au Tv, haiwezi ikawa kimya kimya, lakini kwa sababu ni kimya, ina maana kwamba harakati zimekufa, na mimi siwezi kukaa kimya ndio maana nikaamua kuanzisha The Family", alisema Dkt. John.

Dkt. John amesema mpaka sasa kundi hilo la The Family limefanya nyimbo mbili na zote zikiwa za Hip Hop.