Friday , 28th Feb , 2014

Kundi kongwe la muziki la UB40, linatarajia kutambulisha ujio wake mpya huko Afrika Kusini mwezi April Mwaka huu, likiwa na timu mpya katika bendi ikiongozwa na wasanii watatu Astro, Mickey Virtue na Ali Campbell ambao ni miongoni mwa wanamuziki walioanzisha Bendi hii.

Wasanii hawa wamesema kuwa, tayari wana mzigo mpya wa albam ambayo huenda ikaitwa "Rhythm Method", albam ambayo kwa mujibu wa Ali Campbel imetengenezwa katika ubora ambao hajawahi kuufikia tangu yeye na timu yake walipoanza kufanya muziki.

Wakiwa nchini Afrika Kusini, UB40 watafanya maonyesho kadhaa kuanzia tarehe 4 ya mwezi wa nne na kwa mujibu wa waratibu, kutakuwa na bendi nyingine kali kutoka Afrika Kusini zitakazotumbuiza kwa ajili ya kuongeza ladha zaidi katika onyesho hili.