Saturday , 29th Oct , 2016

Msanii wa vichekesho nchini ambaye kwa sasa anafanya kazi na kundi la Ze Comedy la EATV maarufu kama Mtanga ameiomba serikali isimamie mauzo ya kazi za wasanii kwa kuwa wasambazaji binafsi wanawaonea wasanii jambo ambalo linadidimiza tasnia ya sanaa

Msanii wa kundi la Ze Comedy la EATV ,Mtanga

Mtanga ameyasema hayo katika kipindi cha  SUPAMIX katika programu maalumu inayokwenda kwa jina la ‘KAMATIA KITAA’ ambapo kipindi kilifanyika katika Stendi  ya Morocco Jijini Dar es salaam ambapo kundi la Ze Comedy lilishiriki na kuzungumza na wananchi na kubadilishana mawazo.

“Ninaiomba serikali iingilie kati kusaidia wasanii kwa kuwa tunaumia sana, mfano unaandaa kazi yako ukienda kwa msambazaji anakuambia kaigize na fulani ambaye ni ‘star’ ili tuichukue kazi yako tofauti na hapo hatuitaki kazi yako” Amesema Mtanga

Kufuatia hali hiyo Mtanga amesema ndiyo maana wasanii wengi chipukizi wanakwama kuendelea kwasababu wanakuwa hawana uwezo wa kupata usaidizi wa karibu kutoka kwa wasambazaji binafsi hivyo serikali ikiingilia kati wasanii watafaidi sana matunda ya kazi zao.