Tuesday , 10th Nov , 2015

Msanii Mr. Blue amesema wao kama wasanii inawawia vigumu sana kujibu maoni ya mashabiki kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii, kutokana na wingi wa maoni hayo.

Mr. Blue ameyasema hayo alipokuwa akiongea na timu ya Planet Bongo ya East Africa Radio, na kueleza kuwa kumjibu mtu mmoja mmoja ni ngumu na itaonyesha upendeleo kwa wale ambao wamepata fursa ya kujibiwa.

"Sio muhimu sana kuwajibu wote kwa sababu utakapo mjibu mmoja na mmoja ukamuacha tayari utakuwa umebagua alafu ni kosa, na ukizingatia wengine wanapata comments zaidi ya elfu tano, kwa hiyo sasa huwezi kujibu comments zote hizo, ina umuhimu kujibu lakini kumjibu mtu mmoja mmoja inakuwa kazi sana, ila tunaweza tukawajibu kwa njia nyingine ya kupost kitu kingine na kuonyesha kuwa umepitia comments zao ", alisema Mr. Blue.

Mr. Blue aliendelea kwa kusema kwamba ni muhimu kwa wao kusoma maoni hayo kwani ni muhimu kwa mashabiki kujua kitu kuhusiana na muziki wao.

"Mi naona wakati mwengine ina umuhimu kwa sababu mashabiki wanataka kujua, labda kuna maswali wanataka kukuuliza ya muhimu ambayo yanahusiana na muziki wako, wanataka kujua either unataka kutoa nyimbo mpya au labda kuna nini kipya kutoka kwako, unaweza ukawajibu isiwe labda kwa mmoja mmoja, lakini ni muhimu kusoma comments", alisema Blue.