Sunday , 29th Jan , 2017

Mwanamuziki wa Injili, Christina Shusho amesema hawezi kufanya kolabo na wanamuziki wakubwa wa muziki huo kwa sababu hakuna anachohitaji kutoka kwao na wala yeye hana kitu anachoweza kuwasaidia kwa kuwa wana kila kitu

Christina Shusho

Shusho ametoa kauli hiyo wiki hii alipokuwa akijibu maswali ya watu katika kipindi cha KIKAANGONI ambacho huruka LIVE kupitia ukurasa wa facebook wa EATV, ambapo moja kati ya mashabiki zake walitaka kujua sababu za yeye kutofanya kazi za kushirikiana (Kolabo) na wasanii wengine wakubwa wa muziki kama Rose Mhando, Bahati Bukuku n.k

Katika majibu yake, Shusho alisema lengo la kumshirikisha mtu mwingine kwenye kazi yake ni kama yeye hajiwezi au anataka kusaidiwa kutoka, au kama anataka kumsaidia mtu mwingine kutoka, kwahiyo ameweka nguvu nyingi kushirikiana na wasanii wachanga kuliko wasanii wakubwa wa muziki wa injili.

Alisema kwa hatua aliyofikia sasa anaona anajiweza na hakuna anachohitaji kutoka kwa wasanii wengine wakubwa, huku akisema anachokifanya na atakachoendelea kufanya ni kushirikisha wasanii ambao bado hawajafahamika, ili awe daraja la kuwainua na kuwatoa kimuziki.

"Principle number one kwangu mimi, kwanini nishirikiane na wewe wakati una nguvu ya kutosha inayokupeleka, nataka nifanye kitu nimsaidie mtu, haya mengine ni kama fashion tu kujionesha kuwa nifanya kolabo na fulani, wewe una fan base kubwa, kitu pekee unachohitaji ni Mungu tu, lengo siyo kuimba na mtu, lengo ni kusaidia ule ugumu wa kuanza" Alisisitiza Christina

Christina Shusho akiwa Kikaangoni

Mtu mwingine aliyetaka kujua ni kwani anapenda kufanya kazi na wakenya kuliko watanzania, Shusho alisema kuwa siyo kweli, na kuweka wazi kuwa ni kweli hakuna msanii wa Tanzania aliyeimba naye, lakini wapo wengi hasa wasanii wachanga ambao amewasaidia katika kazi zao ikiwa ni pamoja na kuweka 'back vocals'

Aidha Christina alitumia fursa hiyo pia kuwaonya wasanii wachanga wa gospel ambao wameingia kwenye tasnia hiyo kwa lengo la kutafuta pesa, na kusema kuwa kama kuna mtu anataka kufanya kolabo na yeye kwa lengo la kutafuta umaarufu na kupata pesa, ajitafakari upya

"Kushirikiana na wewe lazima nikusikilize nijue unawaza nini, kuna wengine wanadanga kuwa kwenye uimbaji kuna pesa, sasa kama unataka pesa, usije, mimi sikuanza kuimba kwa ajili ya kutafuta pesa, niliingia kwenye uimbaji kwa ajili ya injili" Alisema Christina.

Pia hakusita kuwataja waimbaji waliomvutia kuingia kwenye uimbaji kuwa ni pamoja na Bahati Bukuku, Rose Mhando, Jenifer Mgendi, Upendo Nkone na Flora Mbasha