Friday , 8th Jul , 2016

Mwanamuziki maarufu wa Marekani Beyonce amewataka Wamarekani kuzuia hasira na mkanganyiko kwa wanasiasa na wabunge wao kufuatia mauaji ya kibaguzi dhidi ya Wamarekani weusi.

Mwanamuziki wa Marekani Beyonce.

Watu maarufu nchini Marekani wamekuwa wakielezea hisia zao kuhusu kisa cha hivi karibuni ambapo polisi walionekana wakimpiga risasi mwanaume mweusi wa Kimarekani.

Kwa upande wa Beyonce amesema ''sote tuna uwezo wa kuonyesha hasira zetu kwa vitendo'', akiwataka Wamarekani kuwasiliana na wanasiasa wao wilayani na kudai haki zap za kijamii na mabadiliko ya sheria.

Beyonce alinyamaza kimya kwa muda wa dakika moja wakati wa onyesho lake mjini Glasgow kuwakumbuka wamarekani wawili waliouawa na polisi kwa kupigwa risasi, na kuweka majina yao Alton Sterling na Philando Castile kwenye screen kubwa huku akitoa wito wa kumalizika kwa ''ubaguzi'' nchini Marekani.

Mumewe Beyonce Jay Z ametoa wimbo mpya kuhusu ufyatuaji risasi. Katika wimbo wake wenye miondoko ya rap Jay Z anahoji kwanini Marekani haibadili sheria yake kuhusu matukio haya ambayo yamezua mjadala mkubwa juu ya ukatili wa polisi nchini Marekani.

Licha ya Jay Z wanamuziki wengine wa Marekani kama Chris Brown, Solange Knowles na Swizz Beatz pia wametoa nyimbo kuhusu mauaji ya kibaguzi nchini Marekani.