Thursday , 20th Sep , 2018

LIVE UPDATES: Ajali ya Mv Nyerere

UPDATE: Septemba 23, Saa 10:10 Asubuhi

Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi Mhandisi Isack Kamwelwe amesema jumla ya miili iliyopatikana hadi sasa katika ajali ya kivuko cha MV. Nyerere imefikia 223.

Aidha, Waziri  Kamwelwe amesema miili 23 ambayo haijapata ndugu zao itazikwa leo katika makaburi ya pamoja.

Shughuli ya uchimbaji wa makuburi inaendelea kwa ajili ya maziko ya miili ambayo haijatambuliwa. Makaburi hayo yanachimbwa mita 250 kutoka gati la Bwisya ambako shughuli za uokoaji bado zinaendelea.

UPDATE: Septemba 22, Saa 2:35 Usiku

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Mwanza Mh. John Mongela, idadi ya waliopoteza maisha mpaka sasa imefikia 218, huku maiti 172 zikiwa zimeshatambuliwa na ndugu zao. Kesho kuanzia saa 2 asubuhi shughuli ya mazishi ya kitaifa itaanza.

Saa 10:50 Jioni Septemba 22

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi Mhandisi Isaack Kamwele hadi sasa miili 209, imeopolewa na watu 41 wameokolewa wakiwa hai.

Kati ya maiti 209, 172 zimetambuliwa wakati 37 hazijatambuliwa na utambuzi unaendelea.

Kati ya maiti 172 zilizotambuliwa 112 zimeshachukuliwa na ndugu.
 

Saa 7:30 Mchana Septemba 22

Mpaka sasa jumla ya miili 47 imeopolewa leo huku zoezi likiwa lnaendelea.

Saa 5:22 Asubuhi Septemba 22

BREAKING NEWS: Mmoja wa Mainjinia wa Kivuko cha Mv.Nyerere kilichopata ajali ya kuzama ziwa Victoria ameokolewa muda mfupi uliopita akiwa hai japo hali yake ni mbaya lakini anapatiwa huduma.

Imeelezwa fundi huyo alikuwa amekwama kwenye moja ya vyumba vya manahodha na alikuwa akigongagonga vitu ili waokoaji wamsikie jambo ambalo limetimia.

Lakini hawezi kuongea kutokana na hali yake kuwa mbaya baada ya kukaa ndani ya maji kwa takribani siku tatu.

Saa 4:30 Asubuhi Septemba 22

Miili mingine minne imeopolewa na kufanya jumla ya miili 26 kuwa tayari imeopolewa leo. Zoezi linaendelea.

Baadhi ya ndugu ambao jana walikataa majeneza ya kuzikia jamaa zao waliofariki katika ajali hiyo, wamebadili maamuzi yao na kuanza kudai wapewe majeneza.

Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania  imetoa mchango wa shilingi milioni 10 kwaajili ya kutengeneza majeneza 100, fedha amekabidhiwa RC Mongella naye kamkabidhi Mhazini. Waziri Jenista Mhagama amesema fedha zitaingizwa kwenye akaunti ya maafa itakayotangazwa.

Saa 2:34 Asubuhi Septemba 22

Miili mingine mitano imeopolewa na kufikisha jumla ya miili 21 kwa siku ya Leo  na kufanya jumla ya miili 157 iliyoopolewa hadi sasa.

Saa 2:20 Asubuhi, Septemba 22

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela amesema Miili mingine 16 imeopolewa na kufanya jumla ya watu 152 waliofariki dunia kwenye ajali hiyo huku akibainisha kuwa zoezi la uokoaji linaendelea 

Aidha amesema kuwa katika zoezi la utambuzi  miili 116 imeshatambuliwa na ndugu zao.

Katika Hatua Nyingine Mongela amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kutolewa  kiasi cha shilingi laki tano kwa kila familia ambayo imepotelewa na ndugu yake kwenye Ajali hiyo.
 

Saa 11:20 Jioni, Septemba 21: Miili yafikia 131, yatambuliwa 36

Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama jana mchana Septemba 20, 2018 imefikia 131 huku uokoaji ukiendelea.

Akizungumza katika kituo cha Afya Bwisya leo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Issack Kamwelwe amesema miili 36 tayari imetambuliwa na ndugu na jamaa wakati kazi ya kuitambua iliyosalia ikiendelea.

Amesema hadi leo mchana waokoaji walikuwa wameipata miili 76 na waliporejea tena kuanzia saa 10 jioni walifanikiwa kupata mingine na kufanya idadi yake ifikie 131 na zoezi litakamilika saa 12 jioni.

Saa 7:00 Mchana, Septemba 21: Miili zaidi ya 125 imepatikana zoezi la uokoaji linaendelea

Mpaka sasa miili zaidi ya 125, imepatikana katika ajali ya kivuko cha MV. Nyerere kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella na zoezi la uokoaji linaendelea

Saa 6:40 Mchana, Septemba 21: Jeshi la Polisi kufungua Jalada la uchunguzi

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Nchini (IGP) Simon Sirro amesema kuwa litafunguliwa Jalada maalum la kuchunguza tukio la kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere jana, Septemba 20 mita chache kabla ya kuwasili katika kisiwa cha Ukara.

IGP Sirro amesema kuwa kwa sasa zoezi la utambuzi wa miili iliyopatikana linaendelea huku pia uokoaji ukiendelea ili kutafuta wengine ambao hawajapatikana.

Saa 5:36  Asubuhi, Septemba 21: Waliofariki wafikia 94

Idadi ya miili iliyopatikana hadi sasa imeongezeka na kufikia 94 zoezi la uokoaji bado linaendelea, hii ni kwa mujibu  wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella

Saa 4:44 Asubuhi, Septemba 21: Waliofariki wafikia 86, chanzo cha ajali chatajwa

Saa zaidi ya 20 tangu kuzama kivuko cha MV Nyerere, idadi ya watu waliokufa imefikia 86, kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella hadi leo saa 4 asubuhi Septemba 21, 2018 jumla ya maiti 86 zimeopolewa .

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cornel Maghembe amesema kuwa sababu ya kuzama kwa kivuko hicho inasadikika kuwa ilibeba watu zaidi ya 400 ambapo kilizidisha uwezo wake ambao ni watu 101.

Maghembe amesema kuwa imezama mita chache kabla ya kuwasili eneo la Ukara ambapo dereva alipunguza mwendo kuashiria amekaribia kutia nanga ndipo abiria wengi walihamia upande wa lango la kutokea wakiwahi kusogea ili washuke ndipo uzito ulizidi na kupinduka.

“Abiria walipoona mwendo umepunguzwa walikimbilia kuwahi mbele ya lango ili kujiandaa kushuka, ndipo uzito ukaegemea upande mmoja”, amesema Maghembe

Saa 3:10 Asubuhi, Septemba 21: Zoezi la Uokoaji linaendelea MV. Nyerere

Baada ya kusitishwa kwa zoezi la uokoaji wa abiria wa ajali ya kivuko cha MV. Nyerere jana jioni baada ya giza kuingia, limeendelea leo alfajiri ambapo hadi sasa waokoaji waliozama majini bado hawajatoka.

Akizungumza na East Africa Radio, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi Jonathan Shana, amesema kuwa tayari kikosi cha uokoaji kimeshaanza uokoaji tangu saa 11 alfajiri ambapo hadi walipositisha zoezi hilo tayari walikuwa wameopoa miili 44 na waliohai 32.

 

Saa 11:00 Jioni , Septemba 20 : Watu 6 wafariki dunia Mv Nyerere

Watu sita wamefariki dunia na wengine 20 kuokolewa baada ya Kivuko cha MV Nyerere  mkoani Mwanza kinachofanya safari kati Bugorora katika Kisiwa cha Ukerewe na Kisiwa cha Ukara katika Ziwa Victoria kuzama leo Alhamis Septemba 20,2018 mchana katika ziwa Victoria.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha amesema timu ya uokoaji bado inaendelea na kazi ya uokozi na kuna uwezekano idadi ya waliofariki dunia ikaongezeka.

Kuna maelezo kuwa katika kivuko hicho kulikuwa na abiria zaidi ya 100 baada ya kupinduka idadi kubwa ya watu wanahofiwa kufariki dunia,” amesema Nyamaha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana amesema kivuko hicho kimezama wakati kikielekea katika Kisiwa cha Ukara.

Kamanda Shana amesema kuwa kivuko hicho kimezama leo mchana baada ya kupinduka. “Kiliondoka saa 6 mchana na ilipofika saa nane kamili mchana kilipinduka,” amesema.

 Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Hassan Karonda amekiri kuzama kwa kivuko hicho Kivuko hicho cha Mv Nyerere kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu.

Mwezi Julai kivuko hicho kilifungwa injini mpya baada ya awali kupata hitilafu na kimekuwa kikitoa huduma kwa watu wa Ukerewe tangu 2004.