Sunday , 12th Apr , 2015

Zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) limeingia katika hatua ya mwisho mkoani Njombe.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania - NEC, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva.

Zoezi hilo lilizinduliwa Februari 24 mwaka huu katika halmashauri ya mji wa Makambako na kisha kuendelea katika halmashauri zote za mkoa wa Njombe.

Uandikishwaji huo unatarajia kumalizika April 15 na kwamba kata zilizo salia kila halmashauri zimeanza kukamilisha uandikishaji ambapo katiaka halmashauri ya mji wa Njombe, kata za Ramadhani na Njombe mjini zilizowekwa kipolo zimeanza uandikishaji.

EATV imepita katika vituo mbalimbali ndani ya kata za Njombe Mjini na Ramadhani hususani vituo vilivyopo mitaa ya Kibena na Idundilanga na kujionea foleni ndefu ambayo bado imeendelea kuzua malalamiko kwa baadhi ya wakazi ambao wanaiomba tume kubadili ratiba ya kufungua vituo kwani wamekuwa wakifika usiku kujiandikisha huku vituo vikifunguliwa saa mbili kama ilivyopangwa.

Lameck Ulaya ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Idundilanga ambao una jumla ya vituo vinne ya kuandikisha ambapo amesema huenda wananchi wakawa na dhamira ya dhati katika kuwapata viongozi wao Kktika uchaguzi mkuu wa Oktoba, kutokana na mwamko mkubwa wa jamii kujitokeza katika vituo vyao pamoja na kuhimiza wananchi wengi kuendelea kujitokeza

Katika kata za Njombe Mjini zoezi hilo linaonekana kuwa na mafanikio makubwa kutokana na tume kuamua kuwatumia waandikishaji kutoka kata nyingine ambao wana uzoefu na mashine za BVR ambapo zaidi ya watu 150 wanaandikishwa katika vituo kwa kila kituo kwa siku.