Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini Tanzania imeanza mpango wa kugawa ramani ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ili kuwawezesha viongozi wa serikali za Mitaa kuondokana na migogoro ya ardhi inayosababishwa na ujenzi holela wa makazi pamoja na uvamizi wa maeneo ya umma, maeneo ya wazi na yale yaliyohifadhiwa.
Akijibu swali la Mhe. Lucy Magereli Bungeni aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kuhakikisha ramani hizo zinafika nchi nzima, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe.Angelina Mabula amesema wizara yake imehakikisha ramani hizo zinawafikia makatibu tawala wa mikoa ili kuionesha kwa wananchi na kuyalinda maeneo hayo.
Kwa upande Mwingine Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani amesema Serikali imesema inatafuta Shilingi Bilioni 19 za kuwalipa wakazi 742 wa Kipunguni waliofanyiwa tathmini ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 1990.
"Wakazi wapatao 1500 wa eneo la kipawa walilipwa fedha zao kiasi cha bilioni 18 katika kipindi cha mwaka 2010, serikali ililipa bil 12 kwa wakazi wa kigilagila zoezi lililokamilika mwaka 2011"alisema
Hadi kufikia mwaka 2011 Serikali imekuwa ikiwalipa wananchi wa Kipawa, Kigilagila na Kipunguni kwa awamu tofauti ambapo zaidi ya wakazi 3,000 wameshalipwa Shilingi Bilioni 31.2