Katika ziara hiyo waziri mkuu amejionea hali ilivyo na kusema kuwa mita hizo za Kurasini zilinunuliwa na serikali kwa gharama za dola za Marekani milioni 1.2 (wakati huo) na haiwezekani kuacha kuzitumia wakati watu wanachezea mifumo na kuongeza mianya ya kupoteza mapato kwa serikali na kuagiza mita hizo zianze kufanya kazi mara moja.
Aidha, Waziri Mkuu amempa saa nne pekee Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita na amletee barua hiyo ofisini kwake ifikapo saa 11 leo jioni.
Pia waziri mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya serikali na kampuni ya Oryx Energies.
Katika ziara hiyo ilibainika kuwa kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu waziri mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.









