
Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba
Waziri Tizeba ametoa kauli hiyo wakati akiongoza mamia ya watu kuaga miili ya watumishi hao watano waliokuwa wakifanya kazi kwenye wizara ya kilimo, akidai maelezo ya polisi yalitofautiana na baadhi ya maelezo ya mashuhuda ambao yeye binafsi alizungumza nao.
Waziri Tizeba amesema “naomba kauli iliyotolewa na jeshi la polisi irudiwe tena waende wakafanye utafiti wa kweli kwani kumekuwa na lawama kwa dereva wa serikali ambazo hazistahili maana taarifa zinasema kuwa dereva wa Lori alikuwa anaingia barabarani pasipo kufuata taratibu jambo lililopelekea kutokea kwa ajali hiyo.”
“Ninaomba sana jeshi la polisi kutenda haki katika tukio hili lenye kuacha maumivu kwa familia, wizara na taifa zima”, ameongeza Dkt Tizeba.
Aidha waziri huyo amewataka jeshi la polisi kutenda haki kwa pamoja na kutoa salamu za pole kwa familia na ndugu pamoja na wafanyakazi wa wizara walioguswa na na tukio hilo la ajali ambalo lilipelekea vifo vya watumishi wa wake.
Watumishi walioagwa kwa kupoteza maisha katika ajali ya gari ni Dereva Mwandamizi wa wizara ya kilimo, Ndg Abdallah Seleman Mushumbusi (53), Afisa kilimo wa Wizara, Ndg Charles Joseph Somi (33), Mkemia daraja la kwanza Ndg Erasto Isack Mhina (43), Mtakwimu daraja la kwanza Bi Ester Tadayo Mutatembwa (36) na Mhasibu daraja la pili Bi Stella Joram Ossano (39).