
Serikali ijayo imetakiwa kuweka sheria ambayo itamfanya kijana kuwa na wasaidizi wa kisheria, ili kuweza kumsaidia kijana pale anapokuwa na uhitaji.
Rai hiyo imetolewa na Mwanasheria Hussein Sengu kutoka kituo cha msaada wa kisheria (LHRC), alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super Mix kinachorushwa na East Africa Radio.
Sengu amesema kwamba asilimia kubwa ya watu wanaoingia katika migogoro ya kisheria ni vijana kutokana na kutokuwa na ajira na kutokuwa na matumaini ya kesho.
"Nimedokeza suala la wasaidizi wa kisheria hapo mwanzo, kwa sababu ni watu ambao wamekuwa na msaada mkubwa sana wa kutoa ushauri wa kisheria, lakini mpaka sasa hivi nchi bado haijatambua na hakuna sheria inawaruhusu kufanya kazi yao vizuri, kulikuwa na mapendekezo mengi kutoka taasisi au asasi zisizo za kiserikali ikiomba serikali ipitishe hiyo sheria, hawa wasaidizi wa kisheria vijana wetu wangeweza kuwa na uelewa wa kisheria, wangeweza kutatua matatizo madogo madog, wangeweza kusaidiana na kuisaidia jamii", alisema Hussein.
Sengu pia ameitaka serikali kuangalia sekta zisizo rasmi kwani ndizo zinazoajiri asilimia kubwa ya wananchi, lakini haina sheria rasmi inayosimamia sekta hizo na kuwawezesha vijana kuendesha maisha yao.
"Liangaliwe suala la sekta isiyo rasmi kwani inaajiri zaidi ya asilimia 80 ya wananchi, mnatengeneza lini sheria ya kuweza kuwatambua hawa watu na kuwawekea mazingira mazuri, sheria nyingi zinahitajika hapa, kuna sheria za masuala ya mikopo, vijana wanashindwa kwenda kukopa kwa sababu taasisi za kukopesha zina riba kubwa sana, nafikiri tukianza na hayo tutaboresha maisha ya vijana", alisema Hussein.