Friday , 3rd Jul , 2015

Waumini wa madhehebu tofauti mkoani Tanga wameanza zoezi la kuliombea taifa katika mchakato wa uchaguzi mkuu ujao ili uweze kufanyika kwa amani na utulivu pamoja na kupata viongozi ambao watajali maslahi ya watanzania.

Baadhi ya waumini wakiwa katika ibada ya kuliombea taifa jijini Tanga.

Wakizungumza katika ibada maalum ya kuliombea taifa pamoja na kuwasimika baadhi ya viongozi wa makanisa mbalimbali wamewataka watanzania kuacha kushabikia vyama na badala yake wachague viongozi ambao wataendelea kudumisha utaifa na kusimamia sera ambazo zitaleta maendeleo kwa taifa.

Aidha askofu wa kanisa la Free Pentekoste jimbo la Tanga mchungaji John Mwakyusa amewataka viongozi wa itikadi za vyama tofauti kutumia vyema majukwaa ya kisiasa katika kampeni zao kutoa lugha ambazo zitakuwa na elimu ndani yake kwa wananchi

Kufuatia hatua hiyo baadhi ya viongozi wakuu wa madhehebu nchini wamewataka baadhi ya viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi mkuu kusimamia na kutekeleza ahadi zao ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wananchi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi ambayo imesababisha maafa katika maeneo tofauti hapa nchini.