Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Rehema Nchimbi.
Serikali imewataka wasimamizi wakuu wa rasilimali watu katika mamlaka za serikali za mitaa kuwajibika na kuhakikisha kuwa watumishi wote wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza katika halmashauri zao wanapatiwa mafunzo elekezi ndani ya miezi sita .
Akizungumza mjini Dodoma Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk, rehema Nchimbi amesema rasilimali watu wenye maarifa na weledi ni muhimu kuliko nyingine zote katika taifa lolote duniani katika kupiga hatua za kimaendeleo.
Dk Nchimbi alibainisha kuwa mafunzo na semina zinazotolewa kwa wasimamizi wakuu wa rasilimali watu katika mamlaka za serikali za mitaa hazijaweza kukidhi matarajio yaliyokusudiwa.
Wakati huo huo, serikali imeanza kuchukua hatua zinazolenga kupunguza matumizi makubwa ya fedha katika taasisi na idara mbali mbali za serikali, kama sehemu ya kukabiliana na nakisi katika bajeti ya mapato na matumizi ya serikali.
Naibu waziri wa fedha na uchumi Mhe. Mwigulu Nchemba, amesema hayo na kutaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuachana na matumizi ya anasa pamoja na kuondoa asilimia tano kutoka kwenye fungu la matumizi mengine ya idara hizo.
Kwa mujibu wa naibu waziri Nchemba, siku chache zijazo wizara yake itakutana na watendaji waandamizi wa wizara na idara za serikali kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na utekelezaji wa mpango wa kupunguza matumizi ambao pia utahusisha kuachana na ununuzi wa magari ya kifahari.