Friday , 24th Aug , 2018

Baada ya Mtandao wa kutuma ujumbe mfupi unaobeba mafaili ya sauti, video na picha mnato 'WhatsApp', kulalamikiwa nchini India kwa kutodhibiti baadhi ya mafaili au taarifa zisizofuata maadili, baadhi ya watumiaji wa mtandao huo nchini, wameeleza kero zinazowakumba.

Picha kivuli ya watu wakiperuzi mtandaoni.

Wakitoa maoni yao kupitia Ukurusa wa FaceBook wa East Africa Television ambapo tuliuliza juu ya hasara au kero apatazo mtumiaji wa mtandao huo, wengi wamependekeza kuongezwa kwa vipengele mbalimbali vinavyoweza kudai ruhusa ya mtumiaji ili kutoa au kupokea taarifa, kadhalika na kuchukuliwa kwa vitu vyao kama picha ya utambulisho 'Profile Picture' na namba ya mtumiaji.

Watumiaji wengine wamelalamikia kutokuwepo kwa mfumo wa kuingia na kutoka kwa kutumia Nywira (Log in na Log Out kwa password).

Pia utaratibu wa mtandao huo kuruhusu watu kwenye makundi yanayoundwa kuongezwa bila ridhaa ya mtu umelalamikiwa, hivyo kuhitaji angalau uwepo utaratibu wa mtu kukubali au kukataa pindi anapoongezwa kwenye kundi.

India kupitia kwa Waziri wa Teknolojia Bw. Ravi Shankar Prasad, wamelalamika juu ya mtandao huo kushindwa kudhibiti au kufuta kabisa ujumbe ambao unakuwa si wa kweli na unasambazwa kwa haraka kwa watu wengi wa eneo moja ambao mwisho husababisha madhara kama vifo.