Manispaa ya Kinondoni imesema kuwa mpaka leo watu watatu wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Kipindupindu na watu wengine 34 wamebainika kuwa na ugonjwa huo kufuatia kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa huo katika Manispaa ya Kinondoni.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dk. Aziz Msuya amesema kuwa mgonjwa wa kwanza aligunduliwa maeneo ya Kijitonyama kwa Ali Maua na alifia nyumbani kwake na kuambukiza ndugu zake wawili ambao walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitali.
Dk. Msuya amesema kuwa kuna kambi za muda katika hospital za Kijitonyama, Mwananyamala na Sinza na kambi kuu ikiwa katika hospitali ya Mburahati, hata hivyo amewataka wananchi wote wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari kwa kuweka mazingira safi, kunywa maji yaliyochemshwa na kujiepusha kula vyakula vilivyopikwa katika mazingira yasiyo masafi na salama.