Saturday , 5th Dec , 2015

Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani amewataka wasomi nchini kuwa mstari wa mbele katika kuitumia elimu waliyoipata vyuoni katika kutetea haki za binadamu.

Jaji Ramadhani ambaye pia ni jaji wa mahakama ya Afrika ya haki za binadamu, ametoa kauli hiyo mjini Dodoma kwenye kongamano la wasomi lililofanyika kwenye chuo kikuu cha St, John’s kwenye mdahalo uliokuwa ukielezea umuhimu wa vyuo vikuu nchini katika kutetea haki za binadamu.

Jaji Ramadahani amesema vyuo vikuu nchini vina umuhimu mkubwa sana kwa kuwa wao ndiyo wana watu wasomi ambao wanaweza kutoka na kuwaelimisha watu wengine, kufanya uchunguzi na kuweka mashinikizo kwenye serikali na kuweza kutekeleza haki vijijini na kusikiliza shida zao na kuzifikisha mahali panapohusika.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya Chuo cha St Johns, Balozi Paul Rupia amesema umuhimu wa suala la haki za binadamu siyo la kuzungumzwa tu ni lazima litekelezwe kama lilivyo kwenye katiba ya nchi.