Saturday , 2nd Jul , 2016

Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini TACAIDS kwa kushirikiana na mgodi wa dhahabu wa Geita GGM unatarajia kupandisha watu 50 katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha fedha ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi nchini.

Mfuko wa kuchangisha fedha hizo ujulikanao kama Kili Challenge kwa mwaka huu umepata washiriki wengi zaidi kutoka nje na ndani ya nchi kwa ajili ya kushiriki upandaji Mlima ambapo watu 50 watafika kilele cha Mlima huo na wengine 50 watauzunguka Mlima kwa muda wa siku mbili.

Akiongea na waandishi wa habari Afisa habari wa mgodi huo Bw. Tenga Tenga amesema imekuwa desturi kwa mgodi huo kuchangia shuguli mbalimbali za maendeleo ya jamii hususan Afya ambapo kwa ugonjwa wa Ukimwi wanaunga mkono serikali kupambana na kuondoa madhara ya ugonjwa huo.

Naye Balozi wa Kili Challenge msanii wa muziki Mrisho Mpoto amesema watanzania wanatakiwa kutambua kwamba mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ni ya kila mmoja hivyo wanapaswa kuunga mkono kampeni hiyo ili kuisaidia serikali kutimiza malengo ya kuwa na maambukizi sifuri.