Wednesday , 7th Oct , 2015

Zikiwa zimebaki wiki mbili na siku chache tu na kampeni zikiwa zimeshika kasi ili Watanzania wapige kura, msanii Darasa ametoa wito kwa wasanii wenzake ambao wanashiriki kwenye kampeni hizo, na kuwataka kuwa makini na wagombea wanaowatumia wasanii

kama sehemu ya kampeni zao.

Darasa ameyasema hayo kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, na kueleza kwamba hiyo ni changamoto kubwa sana kwa wasanii kwani wasipokuwa makini watajikuta wamepata hasara na kuwapa wana siasa faida.

"Ni changamoto kubwa sana hiyo, na inabidi watu watumie akili nyingi wasitengeneze hasara kubwa sana, niseme mfano mzuri yaani usinunuliwe kwa bei rahisi alafu watu wanaokununua ukaenda kuwapa faida, wawe makini sana na hili suala", alisema Darasa.

Pia Darasa amewataka kuchagua kiongozi ambaye atatumikia Taifa vizuri kuliko maslahi yake binafsi, na kuonya kwamba wengi wao wanaowafanyia kazi sasa hivi hawatakuwa nao baada ya uchaguzi.

"Mwisho wa siku watu ambao tunawafanyia kazi sasa hivi, team ambazo tunazifanyia kazi sasa hivi, hazitokuwa timu zetu kweli kesho kesho kutwa, kwa hiyo tuwe makini na hichi kitu, tuangalie mtu gani ambaye atafanya maisha yetu yakachange kiujumla, atatumikia taifa letu vizuri akafanya kazi ya nchi kuliko maslahi yake binafsi kwa hiyo tuwe makini", alisema Darasa.