Monday , 11th Jul , 2016

WATU 4 wamefariki dunia na wengine 27 wamejeruhiwa baada Lori lililokuwa limebeba mzigo wa saruji likitokea jijini Mbeya kwenda Sumbawanga,kupata ajali eneo la Mlima Mbalizi na kuyagonga magari manne na watembea kwa mguu kabla ya kuanguka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Zahiri Kidavashari

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Zahiri Kidavashari alisema kuwa ajali hiyo imetokea Julai 9 majira ya saa 2:00 usiku, akilitaja Lori aina ya Scania lenye namba za usajiri T 215 CLB likiwa na tela lenye namba T 876 CLB, kuwa ndilo chanzo cha ajali hiyo.

Alisema kuwa lori hilo lilifeli breki na kupoteza mwelekeo na likiwa kwenye mwendo mkali dereva alishindwa kulimudu na ndipo likayaparamia magari mengine manne pamoja na watembea kwa mguu kabla ya kupinduka.

Kamanda Kidavashari, alisema kuwa katika ajali hiyo watu watatu ambao ajina yao hayajafahamika walifariki wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali teule ya Mbalizi Ifisi na kwamba mmoja aliyejulikana kwa jina la Philipo Cheyo alifariki wakati akipatiwa matibabu katika chumba cha wagonjwa Magututi katika Hospitali ya Rufaa.

Aliyataja magari yaliyogongwa kuwa ni pamoja na gari lenye namba za usajili T 705 CVK Toyota Coaster ambalo lilikuwa linatokea Tunduma kuelekea Mbeya, T 720 CFH Mitsubishi Pajero ambayo dereva wake hajafahamika na Toyota Canter lenye namba za usajiri T 719 DEH.

Kidavashari alisema kuwa miili ya marehemu watatu imehifadhiwa katika Hospitali ya Ifisi na kuwataka wananchi kwenda kuitambua miili hiyo.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali Teule ya Mbalizi Ifisi, Elimati Sanga, alikiri kupokea majeruhi 22 pamoja na maiti mbili na kwamba majeruhi wengine wawili walifariki wakati wakiendelea kupatiwa huduma hospitalini hapo.

Alisema kuwa watu waliofariki majina yao hayafahamiki wala wanakotokea na kwamba waliofariki wote ni wa jinsia ya kiume na kwamba majeruhi watano waliokuwa wameumia sana walihamishiwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya.

Aliongeza kuwa majeruhi waliolazwa katika Hospitali hiyo wanaendelea vizuri isipokuwa mmoja mwenye jinsia ya kike ambaye hajitambui na hata ndugu zake hawafahamiki.

“Tulipokea majeruhi jumla 22 lakini mmoja alifariki wakati yupo kwenye gari analetwa hapa na wengine wawili walifariki muda mfupi wakati wakipatiwa huduma na hivyo maiti hapa ziko tatu na hawa watu hawafahamiki,” alisema.

“baadhi ya majeruhi walikuwa wameumia sana na hivyo tuliwahamishia katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, lakini kati ya majeruhi tuliokuwa tumebakiwa nao hapa mmoja pekee ndiye hali yake hairidhishi,” alisema Sanga.

Katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, Lucy Elias, aliyekuwa Muuguzi wa zamu alikiri kupokea majeruhi 10 wakiwemo waliopewa rufaa kutoka Hospitali ya Ifisi na kwamba mmoja alifariki wakati alipokuwa anapatiwa matibabu katika Chumba cha wagonjwa mahututi.

Alimtaja marehemu kuwa ni Philipo Cheyo, mwenye umri wa miaka 39 ambaye alifariki kutokana na kuwa alikuwa amevuja damu nyingi na kwamba majeruhi wengine wamelazwa katika wodi namba moja, namba mbili na namba tatu.

Alisema kuwa majeruhi hao wanaendelea vizuri baada ya kupata matibabu japokuwa wana majeraha makubwa.
“Katika Hospitali yetu tulipokea majeruhi 10 wakiwemo watano waliotoka Ifisi, lakini mmoja ambaye alikuwa ameumia zaidi alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi na alifariki usiku huohuo wakati matibabu yanaendelea,” Alisema muuguzi huyo wa zamu.

Baadhi ya majeruhi waliokuwa kwenye Coaster walisema kuwa ajali hiyo ilitokea wakati Dereva alipokuwa anasimamisha gari sehemu ambayo hairuhusiwi kwa ajili ya kushusha abiria na ndipo lori hilo lilipowavamia.

Mmoja wa majeruhi hao, Isaka Mwaigaga, alisema kuwa dereva wa coaster aliyokuwa amepanda kutoka mjini Tunduma alikuwa anataka kusimamisha gari nje Stendi kwa ajili ya kushusha abiria waliokuwa wanashukia Mbalizi ndipo wakajikuta lori limewavamia.

Alisema kuwa yeye aliumia jicho lakini alikuwa anajitambua hali iliyomfanya kukodi pikipiki kwenda Hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu.