Thursday , 20th Sep , 2018

Baada ya Mahakama ya Afrika Mashariki kutupilia mbali kesi ya kupinga Muungano hapo jana Septemba 19, 2018, walalamikaji wameshauriwa kuwasilisha upya madai yao katika mahakama za Zanzibar.

Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere akichanganya mchanga wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume na mashuhuda wengine April 26, 1964.

Msemaji mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas, amethibitisha kuwa, jopo la majaji limewashauri walalamikaji kuwa wanaweza kuwasilisha madai yao upya katika Mahakama za Zanzibar.

Aidha Dr. Abbas, ameongeza kuwa sababu za kina za uamuzi huo wa kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo zitatolewa baadae.  Katika kesi hiyo, Serikali ilitetewa na jopo la mawakili wakiongozwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi.

Wanzanzibar 40,000 wakiongozwa na Rashid Salum Adiy, walifungua kesi hiyo tarehe 25/10/2016, katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) kupitia Masijala ndogo ya mahakama hiyo iliyoko jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo wadaiwa walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.