Rais Jakaya Kikwete
Wananchi wa vijiji mbalimbali katika wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro wameitaka serikali kuharakisha utekelezaji wa maazimio ya bunge ya kuwawajibisha watu wote waliohusika na wizi wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow ili iwe fundisho kwa watumishi wa umma wanapopewa nafasi za kusimamia majukumu mbalimbali ya serikali.
Wakiongea na EATV wananchi hao wakiwemo vijana wanaojishughulisha na shughuli za uchomaji na uuzaji wa mkaa katika vijiji vya Mikumi, Doma na Mvomero wamesema kitendo cha watu wachache kugawana fedha nyingi kiasi hicho huku wananchi wa vijijini wakiendelea kutaabika na hali ngumu ya maisha kutokana na ukosefu wa ajira na uduni wa huduma muhimu za kijamii kimewakera wananchi wengi wenye uchungu na rasilimali za nchi zikiwemo fedha za umma.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikundi cha vijana wauza mkaa cha Doma Adam Saidi Ali amesema wananchi wanashangazwa na ukimya wa serikali katika jambo hilo nyeti na kwamba kuchelewa kutolewa adhabu kwa wahusika kunajenga taswira kwamba viongozi wa serikali wakikosea huchelewa kuadhibiwa wakati wananchi wa vijijini adhabu zao hutolewa haraka ikishabainika kama kosa limefanyika hata kama ni la wizi wa kuku au kujihusisha na uvunaji wa miti kwaajili ya kuchoma mkaa.
Aidha baadhi yao wamesema wizi wa fedha hizo umewashangaza wananchi wengi kwani kama fedha hizo zingeweza kugawiwa vijijini zingesaidia katika harakati za maendeleo ya wananchi na kuondoa umasikini kwa wananchi walio wengi na pia zingewafanya vijana wengi kuachana na biashara ya mkaa ambayo imekuwa chanzo cha uharibifu wa misitu katika maeneo mbalimbali nchini.