Saturday , 2nd May , 2015

Serikali mkoani Njombe imewataka wakazi wa mkoa huo kuhakikisha wanajitoikeza kwa wingi kupigia kura Katiba Pendekezwa kama walivyojiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Njombe, Sarah Dumba wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi ambapo wafanyakazi mkoani Njombe wameungana na wafanyakazi kote duniani kuadhimisha siku hiyo.

Dumba amesema kuwa wananchi na wafanyakazi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuipigia Katiba Pendekezwa kura ya ndio itakapo tangazwa siku ya kuipigia kura.

Kwa upande wao wafanyakazi wamesema ili kuboresha maendeleo ya mkoa ni vyema miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, mabweni na hospitali ikakarabatiwa.

Akisoma taarifa ya wafanyakazi kwa mkuu wa wilaya katibu wa chama cha walimu wilaya ya Njombe Salama Lupenza alisema kuwa ili mkoa kupata maendeleo unahitajika kuwa na wasomi na kuwa mkoa huo una wajibu wa kuhakikisha unajenga mabweni kwa shule zake ili kuendeleza kushika nafasi za juu kielimu kama ulivyofanya mwaka huu.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika halmashauri ya Njombe kimkoa na kuhudhuriwa na mamia ya wafanyakazi kutoka wilaya mbalimbali wa mkoa huo wafanyakazi wameitaka serikali kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi ili kuweza kuyamudu maisha.