Friday , 17th Jun , 2016

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muunganpo wa Tanzania Majaliwa Kassim amevitaka vyombo vya habari nchini kuendelea kuhabarisha umma kuhusu matukio mbalimbali hasa sehemu zisizofikika ili serikali na wadau waweze kufahamu.

Majaliwa ameyasema hayo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Martha Mlata aliyetaka kujua mkakati wa serikali wa kuwabaini watu ambao wana matatizo ya kiafya na wapo ndani ya jamii ili waweze kupatata matibabu kuliko kusubiri hadi vyombo vya habari kuwafikia kwa vipindi maalumu jambo ambalo linakosesha wengi haki ya kupata matibabu.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema serikali inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kufika sehemu zisizofikika na viendelee kufanya hivyo na serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wote wenye kisukari, kifua kikuu, mama wajawazito, wazee na watoto bure katika hospitali za serikali.

''Serikali imeandaa utaratibu wa kusaidia matibabu nchini kwa kutumia mfuko wa afya pamoja na mfuko wa afya wa watumishi kazini ili kusadia watanzania walio wengi.

Aidha Waziri Mkuu ameahidi kwamba serikali itaendelea kusaidia kuboresha bajeti za wizara za afya ili wizara hiyo iweze kuhudumia wananchi ipasavyo.