Wanafunzi Wa Chuo Kikuu Cha Dodoma Kitivo Cha Sayansi Ya Jamii Na Lugha Wakusanyika Kusikiliza Maelekezo Kutoka Kwa Raisi Wa Chuo Kikuu Cha Dodoma
Akizungumza na East Africa Radio kwa njia ya simu makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Idriss Kikula amesema ameshapata fedha za wanafunzi hao na kwamba hiyo jana alikuwa njiani kurejea Dodoma na fomu za kujaza ili wanafunzi hao waanze kugawiwa fedha zao.
Alisema kuwa baada ya kuona wanafunzi hao wanagoma kuingia madarasani na kufanya maandamano kufuatia kucheleweshewa fedha zao za kujikimu aliamua kufuatilia suala hilo hadi ofisi za bodi ya mikopo ya elimu ya juu Dar es salaam.
Kwa upande wake Rais wa serikali ya wanafunzi, Fredrick Lutelano amewataka wanafunzi hao kuwa watulivu wakati suala lao likishughuliwa na serikali kwani hata kama wakigomea kuingia madarasani chuo hicho hakina uwezo wa kuwalipa.
“Wanapofanya maandamano ni lazima wajuwe wanakabiliana na nani hata kama wakigomea kuingia madarasani chuo hakina uwezo wa kuwalipa fedha zao chuo ni kama daraja tu la kupitishia fedha zao lakini uwezo wa kuwalipa wanafunzi hao hakina,” alisema Lutelano.
Katika maandamano ya jana polisi walilazimika kuingilia kati na kutuliza ghasia ambapo waliweza kuyadhibiti maandamano ya wanafunzi hao kutofika katika utawala mkuu wa chuo hicho.
Maandamano hayo yanafanywa na wanafunzi wa kitivo cha elimu tu, kwani vitivo vingine vimeshaingiziwa fedha za kujikimu.. kwa mujibu wa Rais wa chuo cha Udom, Fredrick Lutelano.