Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mwenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Ali Mohammed Shein, wakionyesha juu Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Masuala hayo ni pamoja na kusogezwa karibu na wananchi, kwa huduma muhimu kutoka jijini Dar es Salaam zinakotolewa hivi sasa hadi katika ngazi ya wilaya.
Wakizungumza katika mkutano wa kujadili katiba inayopendekezwa, wawakilishi wa wakulima wamesema pindi itakapofika wakati wa utungaji wa sheria ndogo ndogo, basi bunge lipewe nguvu ya kutunga sheria itakayosaidia kusogeza huduma hizo muhimu ikiwemo ile ya ukataji wa leseni.
Wafugaji kwa upande wao wameiomba serikali iwatambue kama kundi maalumu kwa kuwa wao ni moja kati ya makundi yanayokuza uchumi wa nchi na kushukuru kwa katiba inayopendekezwa kwa kuona umuhimu wao kuingizwa katika katiba hiyo.
Wakati huo huo, wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema tatizo la ongezeko la migogoro ya ardhi linaloendelea maeneo mbalimbali nchini linachangiwa na ukiukwaji wa sheria unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakitumia umasiki na uelewa mdogo wa wanananchi na kupora ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji.
Akizungumza katika kikao cha kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo katika wilaya ya Monduli Jijini Arusha, Naibu kamishana wa Ardhi Kanda ya Kaskazini Bi. Doroth Wanzala amewataja watendaji hao kuwa ni wale wa ngazi za juu na wa halmshauri ambao badala ya kufata sheria wamekuwa wakiwalaghai wananchi na kuuza ardhi na mara nyingine kuwapora kwa kisingizio cha Uwekezaji.
Bi. Doroth amesema katika kukabiliana na tatizo hilo, wizara inaendelea kuchukua hatua za kutoa elimu pamoja na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuepuka vishawishi vinavyotolewa na baadhi ya watumishi wa umma waliojigeuza mawakala wa wawekezaji, vya kuuza ardhi kwa tamaa ya fedha.