Thursday , 18th Jun , 2015

Wakazi wa Mkoa wa Dodoma wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kufika katika mkoa huo na kutatua migogoro ya ardhi inayowakabili.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Ombi hilo limetolewa na Chifu wa ukoo wa Wanyanzaga kutoka kabila la Wagogo, Lazaro chihoma kwenye ibada ya mitambiko iliyofanyika katika kisima cha Bwibwi kilichopo katika Kata ya Iyumbu, Manispaa ya Dodoma kisima ambacho kina historia ya ukoo huo.

Chihoma amesema ni muda sasa wa waziri Lukuvi kufika katika maeneo ya Mkoa wa Dodoma na kutatua migogoro ya ardhi ambayo mingi inasababishwa na Mamlaka ya Ustawishaji wa makao makuu (CDA).

Amesema kuna maeneo mengi ya kihistoria ambayo yamepotea kutokana na CDA kutowashirikisha wakazi wa mkoa huo na hivyo kuifanya historia ya mkoa wa Dodoma kupotea.

Ameiomba serikali kuyatambua maeneo yenye historia nchini na kuyahifadhi kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Iyumbu uliopo kata ya Iyumbu, Manispaa ya Dodoma, Steven Daudi ameiomba serikali kulitenga eneo la kisima hicho ambacho hutumika kwa ajili ya ibada za mitambiko kwa watu wa ukoo Wanyanzaga ambao idadi yao inafikia watu 817.