Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha (SSP) Emmanuel Tille akiongea na viongozi wa kata ya Moivaro tarafa ya Suye pamoja na askari wa vikundi vya ulinzi shirikishi wakati wa uzinduzi wa vikundi vinne vya kata hiyo
Akizindua vikundi hivyo ambavyo vimewezeshwa na wadau Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mratibu Mwandamizi wa Polisi Emmanuel Tille kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha alisema kwamba matarajio ya wananchi katika kata hiyo ya Moivaro ni makubwa na ana imani watakuwa wanalala na kuamka salama hivyo kuwataka walinzi hao wawe na nidhamu kwenye kazi yao.
“Kazi ya ulinzi ina miiko yake; kitu cha kwanza ni nidhamu ya hali ya juu. Mimi mwenyewe mpaka nafikia hatua hii ni kwa sababu ya nidhamu na nawataka ninyi muige mfano wangu, ninachosema hapa ni pamoja na kuwahi kazini, kutunza siri pasipo kuwazunguka wenzako pamoja na kufuata maelekezo ya wakubwa wa vikundi vyenu” Alisisitiza Tille.
Alisema japokuwa askari hao wapatao 42 wamepewa mafunzo lakini kupitia Wakaguzi wa Polisi wa Tarafa na askari kata wataendelea kuwapa mafunzo mara kwa mara ili waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria, huku akiwaonya wasijichukulie sheria mkononi.
Aliwataka wananchi wanapopata taarifa watoe kwa viongozi wa Polisi mara moja ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka na hatimaye kufikia malengo ya kupunguza uhalifu ndani ya jiji la Arusha, huku akiwataka watendaji wa kata na Wakaguzi wa tarafa wahakikishe askari wa kata wanakuwa katika maeneo yao kila siku hali ambayo itawasaidia kubaini maeneo tete.
Akiongea katika uzinduzi huo Diwani wa kata hiyo Rick Moiro alivitaka vikundi hivyo kufuata taratibu za kazi na kupambana na uhalifu hasa vijana wanaojihusisha na madawa ya kulevya aina ya bangi huku akiomba Jeshi la Polisi litoe ushirikiano wa karibu na vikundi hivyo pindi tu wanapoomba msaada.
Naye Afisa Mtendaji wa kata hiyo Bi. Editha Kisangia alisema kwamba mbali na hali ya uhalifu kuwa ya kawaida katika eneo hilo lakini hatarajii kutokea kwa changamoto kutoka kwa baadhi ya wananchi kushindwa kuchangia vikundi hivyo kwani faida wataiona baada ya kuanza kufanya kazi.
Wakaguzi wa Polisi wanaoongoza tarafa tatu za halmashauri ya jiji la Arusha toka mwaka 2013 ni pamoja na Frimina Massao tarafa ya Suye, Winibrita Moshi tarafa Elerai na Shabani Shabani tarafa ya Themi.


