Wahamiaji haramu wakiwa chini ya uangalizi wa maafisa wa Idara ya Uhamiaji (Picha na Maktaba).
Akizungumzia tukio hilo Afisa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa, Seleman Kamea, amesema watu hao walikuwa wakisafiri ndani ya basi lililokuwa linatokea mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa kwenda mji wa Tunduma, mkoani Mbeya.
Bw. Kamea amesema baada ya uchunguzi wakabaini kuwa hati za usafiri za raia hao kutoka nchini Congo watu wazima wapatao nane na watoto wao 11, walikuwa hawana hati za kusafiria na hivyo kuwakamata na kuwarudisha nchini kwao kupitia njia waliyoingilia.
Aidha, Afisa uhamiaji huyo amesema kuwa watoto waliokutwa katika gari hiyo mwenye umri wa chini kabisa ni mtoto wa mwaka mmoja huku aliekuwa mkubwa zaidi ni miaka 12 ambao wote walikuwa na wazazi wao.
Pia, Kimea amesema kuwa Idara ya uhamiaji mkoani humo imejipanga vizuri katika kudhibiti suala la uhamiaji haramu ikiwemo kutoa elimu kwa wahusika wa usafirishaji kutoka mipakani kuweza kuwahoji abiria ambao wanawatilia shaka kuhusu uraia wao.
Kwa upande wao baadhi ya wahamiaji hao walipohojiwa juu ya safari yao walisema kuwa hawakuwa na nia ya kukaa Tanzania, bali walifanya njia kuelekea nchini Zambia na baadaye nchi nyingine za kusini kutafuta maisha.