Friday , 10th Oct , 2014

Wakazi wa manispaa ya Sumbawanga wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara wa soko kuu, wameifunga barabara yenye shughuli nyingi ya Sokoine kwa kumwaga taka ngumu kwenye barabara hiyo.

wafanyabiashara hao wamechukua hatua hiyo kuonesha hasira zao baada ya kuona lundo la taka hizo likiwa limewekwa pembeni mwa barabara karibu na soko hilo, kwa siku Tano bila ya kuzolewa na kusababisha kero kubwa na kuhatarisha afya zao.

Wakizungumza kwenye maeneo ya soko kuu hilo la mji wa sumbawanga mkoani Rukwa, baadhi ya wakazi wa manispaa hiyo wamesema wanashangazwa na kitendo cha kulundikana kwa taka ngumu hizo bila ya kuzolewa tena chini ya transfoma ya umeme, huku wakitozwa ushuru kila siku kwa ajili ya masuala ya usafi, na huku manispaa ikiwa imepata hivi karibuni malori mawili makubwa ya kuzoa taka ngumu.

Kwa upande wao baadhi ya madiwani wa manispaa hiyo ya Sumbawanga, akiwemo Diwani wa kata ya Mazwi lililopo katika soko kuu hilo Bw. Joseph Ngua, licha ya kukerwa na kitendo cha wananchi hao kumwaga taka ngumu Barabarani na kusababisha usumbufu mkubwa kwa saa kadhaa, wamesema suluhu ni kufanya juhudi kubwa ya kuziondoa taka ngumu hizo mahali hapo, na kwenda kuzimwaga kwenye dampo kubwa.