
Teknolojia hiyo inayofanya kazi kwa njia ya mawasiliano ya setilaiti, inamwezesha mmiliki wa gari kufahamu matumizi ya mafuta, muda unaotumika, picha ya dereva na mahali gari ilipo kwa lengo la kumwezesha kujua kiwango na sababu za gharama anayotumia kama anavyoeleleza Mkurugenzi Uendelezaji Biashara kutoka taasisi iliyobuni teknolojia hiyo Bw. Ebenezer Msuya.
“Suala la gharama za usafirishaji na usalama wa mizigo na magari nchini hivi sasa limeimarishwa kutokana na ujio wa teknolojia hii inayofanya kazi kwa njia ya satelite...anachotakiwa kufanya mmiliki wa chombo cha moto ni kufunga kifaa maalumu kitakachokuwa kinafuatilia mwenendo mzima wa gari husika kwa lengo la kupata taarifa zote muhimu,” amesema Bw. Msuya.
Kwa mujibu wa Bw. Msuya, teknolojia hiyo itasaidia pia kukabiliana na wizi na uchakachuaji wa mafuta, maarufu kwa jina la kupiga nyoka ambapo mmiliki wa chombo chochote cha moto yakiwemo majenereta ya kuzalisha umeme kwenye maofisi na katika nyumba za makazi.
“Hata wezi wa mafuta hivi sasa hawana nafasi kwani kwa kutumia teknolojia hiyo, utaratibu mzima wa uwekaji na matumizi ya mafuta utakuwa ukifuatiliwa hadi kwenye jenereta za kuzalisha umeme majumbani,” amesema Bw. Msuya.
Mbali ya ufuatiliaji wa mwenendo wa magari, teknolojia hiyo pia inaweza kuzuia vitendo vya utekaji na wizi wa watoto kwani mzazi anaweza kufunga kifaa hicho kwenye nguo au begi la shule la mtoto na kufuatilia mwenendo mzima wa mahali alipo mtoto wake kwa lengo la kumlinda.