Tuesday , 25th Aug , 2015

Kundi la watu zaidi ya 100 wakiwa na silaha mbalimbali za jadi wamevamia kituo kidogo cha polisi cha Mbingu, kilichopo wilayani kilombero Mkoani Morogoro na kukichoma kwa moto, wakishinikiza kukabidhiwa mtuhumiwa aliyedaiwa kumuua mkewe ili wamuue.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro Leonard Paulo akiongelea tukio la kuchomwa kwa kituo cha Polisi.

Tukio hilo lililothibitishwa na polisi limetokea saa chache baada ya mtuhumiwa Bashiri Ernest Kadugula kufikishwa kituoni hapo akikabiliwa na tuhuma za kumuua mkewe,Veronica Chambula kwa kumkatakata kwa panga,baada ya kutokea tofauti baina yao.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro Leonard Paulo amesema polisi walifanikiwa kumtorosha mtuhumiwa aliyekuwa akitafutwa, sambamba na baadhi ya silaha, kabla ya wananchi hao kukivamia na kukiteketeza kwa moto kituo hicho cha polisi na kusababisha pikipiki tano zikiwemo mbili za askari polisi, kuteketea.

kufuatia tukio hilo, wananchi wa mkoa wa morogoro wamelaani matukio ya waanchi kuvamia vituo vya polisi na ofisi nyingine za serikali, kuzichoma moto na hata kusababisha hasara mbalimbali.