Tuesday , 14th Oct , 2014

Viongozi walioko madarakani wametakiwa kuwa wazalendo na kumuenzi hayati baba wa taifa kwa vitendo katika kuhakikisha raslimali zilizopo hapa nchini zinawanufaisha watanzania badala ya watu wachache.

Hayo yamebainishwa na wasomi wa chuo kikuu cha Ushirika Moshi wakati wa mdahalo wa kumbukumbu ya miaka 15 ya kifo cha hayati baba wa taifa wa kujadili hali ya Tanzania ilivyo kwa sasa.

Wamesema ni vema watanzania wakamuenzi hayati baba wa taifa kwa vitendo na kuacha mambo ya rushwa na ufisadi ambavyo vinaonekana kulikumba taifa na kuwafanya watu wachache kujinufaisha na raslimali zilizopo hapa nchini.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha wanataaluma wa chuo kikuu cha ushirika Moshi prof. Suleimani Chambo amesema watanzania wengi hususani viongozi wanamuenzi hayati mwalimu nyerere kwa maneno na siyo vitendo kwa kuwa wengi wao ni wabinafsi jambo ambalo ni hatari vya vizazi vijavyo.

Nao baadhi ya wahadhiri wamesema ni vema masomo ya stadi za maisha na elimu ya kujitegemea ikawekwa katika mitaala ya elimu ili kuwaandaa wanafunzi kupenda kujitegemea na kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini.