Sunday , 13th Jul , 2014

aadhi ya maaskofu na wachungaji wa makanisa ya kipentekoste na Sabato nchini Tanzania wamejikuta wakiingia katika mjadala wa umri pamoja na nani anafaa kugombea katika uchaguzi mkuu ujao.

Waziri wa nchi, ofisi ya rais Mahusiano na Uratibu Mhe. Stephen Wassira.

Baadhi ya maaskofu na wachungaji wa makanisa ya kipentekoste na Sabato nchini Tanzania wamejikuta wakiingia katika mjadala wa umri pamoja na nani anafaa kugombea katika uchaguzi mkuu ujao huku wakielezea namna kanisa linavyokerwa na vitendo vya ufujaji mali za umma unaofanywa na viongozi wasio waadilifu.

Katika mkutano wao na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wachungaji hao wamesema kanisa linataka mgombea wa umri wowote kuanzia miaka thelathini ambayo kiimani ndiyo umri ambao Yesu Kristo alianza kuwatumikia wanadamu na kwamba busara na hekima havina uhusiano na umri, kama anavyoeleza askofu mkuu wa kanisa la Jesus Power Miracle Church, askofu Joachim Peter.

Kwa mujibu wa askofu Peter, kuna haja ya vijana kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za juu za uongozi kama ambavyo baadhi wameanza kuonyesha njia huku akionyesha namna nchi inavyohitaji vijana waadilifu kwa ajili ya kulisaidia taifa kukabiliana na changamoto za kiuongozi na maadili.

Kauli ya wachungaji hao imekuja siku chache baada ya mwanasiasa mkongwe mzee Stephen Wassira kudai kupinga kauli aliyoitoa jaji mstaafu Joseph Warioba kuwa nchi inahitaji viongozi vijana aliodai kuwa wana uwezo wa kutosha wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi.

Aidha siku chache baadaye, mbunge wa Musoma Vijijini Mhe. Nimrod Mkono na yeye akaibuka na kusema kuwa anaamini vijana nchini bado hawajakomaa na kuwa na uwezo wa kuongoza na kwamba Tanzania kwa sasa bado inahitaji hekima na busara kutoka kwa viongozi na wanasiasa wazee.