Wednesday , 19th Aug , 2015

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa amewataka viongozi wa dini nchini kuwa mstari wa mbele katika kuwafundisha waumini wao kujiepusha na vitendo vya rushwa katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh. Chiku Gallawa

Gallawa ametoa wito huo leo wakati akizungumza na viongozi wa dini mkoani Dodoma kwenye kikao cha mashauriano kuhusu amani kuelekea uchaguzi mkuu, kilichowakutanisha viongozi wa dini za kikristo na kiislam kilichofanyika mjini Dodoma.

Amesema katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu vitendo vya rushwa vimekithiri miongoni mwa wananchi pamoja na wagombea hali inayohatarisha amani ya nchi hasa kwa wale wanaotaka rushwa kwa nguvu.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu amewataka viongozi wa dini kuwa makini na kauli zao katika kipindi hiki ili kuepusha machafuko ya amani ambayo yanaweza kusababishwa na kauli wanazozitoa kwa kisingizio cha kutumwa na Mungu.