
Akiongea na waandishi wa habari mmoja wa wakazi wa Kata hiyo Mussa Mohamed amesema anashangazwa na kitendo cha serikali kutopeleka umeme katika jengo hilo la kituo hicho cha afya ambalo limejengwa kwa msaada wa Mfuko wa Benki ya Dunia.
"Hili jengo limejengwa kwa ajili ya upasuaji na Mfuko wa Benki ya Dunia, lakini cha ajabu ni kwamba serikali imeshindwa kuweka kipaumbele cha kuleta umeme kwa ajili ya kuhudumia jengo hili na wananchi waendelee kupata huduma zinazostahili," alisema Mohamed.
Mkazi huyo aliendelea kwa kusema kituo hicho ndicho kinachotumika kama hospitali ya wilaya kwani wilayani hapo hakuna hospitali ya wilaya, lakini anashangazwa na kitendo cha kuweka jenereta ambalo lina gharama kubwa kuliko umeme wa kawaida ambao bado haujafika hospitalini hapo.
"Mbaya zaidi wilaya ya Uyui hatuna hospitali ya wilaya, inayohesabika kama hospitali ya wilaya ni hiki kituo cha afya, lakini hakina huduma za umeme mpaka hivi leo, na ukiangalia umbali wa kutoka hapa hadi barabara kubwa ambako nguzo zinapita hazizidi nguzo thelathini, sasa sijui serikali inakuwa na mtazamo gani, benki ya dunia imetupa jengo lenye thamani ya mamilioni na vifaa vya mamilioni, ambavyo vinastahili kuendeshwa kwa kutumia umeme, matokeo yake imekuja kufungwa jenereta ambalo litagharimu fedha nyingi zaidi, mzunguko wa lile jenereta kwa saa ni lita 60," alisema Mohamed ambaye ni mkazi wa wilaya ya Uyui.
Kwa upande waganga wa Kituo hicho Dkt. Edson Shimwela na Said Haji, wamekiri kuwepo kwa tatizo hilo ambalo wameshalitolea taarifa kwa wahusika lakini halijapatiwa ufumbuzi, huku wakisema hulazimika kuwapeleka wagonjwa kwenye hospitali ya Kitete, ambapo muda mwengine hupoteza maisha wakiwa njiani.