Wednesday , 16th Sep , 2015

Ukosefu wa ufanisi wa kiuchumi na kiutendaji kwa baadhi ya mashirika na taasisi za umma umesababisha serikali kuingia hasara kubwa kwa kukopa pesa za kiendeshea mashirika na taasisi hizo.

Msajili wa hazina Bw. Lawrence Mafuru

Msajili wa hazina Bw. Lawrence Mafuru, amesema hayo leo wakati waziri wa nchi ofisi ya rais Profesa Mark Mwandosya, alipokutana na watendaji wa mashirika ya umma yanayosimamiwa na msajili wa hazina.

Kwa mujibu wa Mafuru, fedha zinazoingizwa na baadhi ya mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara, zinaweza kutumika kuboresha huduma za kijamii badala ya serikali kulazimika kukopa pesa kutekeleza huduma hizo au wakati mwingine hata kuendesha mashirika husika.

Kwa upande wake, Profesa Mwandosya amewataka watendaji wa taasisi zilizo chini ya msajili wa hazina kutambua umuhimu wa kujijenga uwezo wa kujiendesha ili kutimiza malengo ya uanzishwaji wake badala ya kuwa mzigo kwa serikali.