
Waziri wa Afya, ustawi wa jamii jinsia wazee na watoto nchini Tanzania Ummy Mwalimu amesema Matukio ya ubakaji watoto nchini yameongezeka kutoka watoto 422 mwaka 2014, kufikia matukio 2,358 mwaka jana.
Ayalisemwa hayo alipokuwa akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa kila ifikapo juni 16 kila mwaka.
Ummy alisema kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2016, matukio 1,765 yaliripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Katika Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam afisa Habari wa Manispaa hiyo Bi Tabu Shaibu amesema kuwa kuanzia mwaka 2013 jumla ya matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yapatao 1,213 yameripotiwa katika kituo cha Amana Hospitali huku matukio ya ubakaji yakiwa 469 yakifuatiwa na matukio ya kulawitiwa.
Hata hivyo ametoa wito kwa jamii kutoa taarifa na kufika katika vituo vya huduma ikitokea kuna ukatili wa kijinsia umejitokeza lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa matukio kama hayo yanatokomezwa kabisa.