Thursday , 12th Feb , 2015

Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imetangaza kusogeza mbele zoezi la uandikishwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR kutoka Februari 16 hadi Februari 23 mwaka huu

Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imetangaza kusogeza mbele zoezi la uandikishwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR kutoka Februari 16 hadi Februari 23 mwaka huu, ili kutoa fursa kwa vyama vya siasa kuteua mawakala watakaokuwepo katika zoezi hilo.

Tume hiyo pia imesema zoezi hilo litaanzia katika mkoa wa Njombe badala ya mikoa minne iliyokuwa imepangwa awali.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa zoezi hilo litaanza huku Tume ikiwa imejiridhisha na hatua walizozichukua dhidi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa majaribio ya uandikishwaji iliyofanyika katika majimbo matatu ya Mlele, Kilombero na Kawe.

Amesema Tume ilikubaliana na serikali kuagiza BVR Kits 8,000 ambapo kati ya hizo ni Kits 250 pekee zilizokwishapokelewa, na kwamba BVR Kits 7750 zinataraji kupokelewa 16/03/2015.

Amesema vituo vya uandikishaji vimeongezeka kutoka 24,919 hadi 36,109.

Kwa upande wao viongozi wa vya siasa nchini Tanzania wameitupia lawama tume hiyo kwa kutokuwa wawazi wa namna ya uendeshaji wa tume hiyo na mchakato mzima wa uiandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Kielectronic BVR.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, viongozi wa vyama vya siasa wakakubaliana na tarehe iliyotangazwa na tume lakini kwa masharti ya kuendesha zoezi hilo kwa uwazi na ueledi kama miongoni mwa maazimio.

Wamekubalina kuwa Tume ya Uchaguzi pamoja na NIDA kila moja itaendelea na kazi zake kama ilivyojipangia.

Azimio lingine ni kwamba mfumo wa BVR utumike kwenye uandikishaji pekee na siyo wakati wa kupiga kura, pia wamekubaliana kuwa vifaa vinavyotumiwa na Tume baada ya zoezi vikabidhiwe kwa mamlaka ya vitamubulisho vya taifa NIDA kwa ajili ya kuharakisha zoezi ya vitambulisho vya Taifa.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, vitambulisho vya Taifa vitaweza kutumika katika upigaji kura na vitamuwezesha mtu kuchagua Rais akiwa sehemu yoyote Tanzania.

Tume imewahakikishia viongozi wa vyama vya siasa kuwa zoezi hilo litamalizika kabla ya April 30 mwaka huu.