Wednesday , 15th Apr , 2015

Kiongozi mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema kuwa serikali imewadanganya wananchi wa Tanzania kuwa itahamishia makao makuu yake Mkoani Dodoma adhma ambayo haijatekelezwa hadi sasa.

Kiongozi mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe.

Zitto ametoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati akihutubia maelefu ya wananchi wa mji huo wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya mashujaa mjini hapa.

Amesema japo serikali imekuwa ikipiga kelele kila siku kuhusu kuhamishia makao makuu yake katika mji wa Dodoma lakini kauli hiyo imekuwa haina vitendo kutokana na uhalisia wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi kutofanya hivyo.

“Lakini nataka niwahahakikishie Watanzania kuwa Chama cha ACT-Wazalendo kitakapoingia madarakani, Rais wake ataapishiwa katika uwanja wa Jamhuri na si uwanja wa Taifa pale kwenye shamba la bibi ambapo huwa anaapishiwa, ambapo mawaziri wake wataapishwa katika ikulu ya Chamwino,” alisema Zitto.

Amesema kutokana na serikali kushindwa kuhamishia makao makuu yake mjini Dodoma, mkoa huo umeendelea na hali ya umaskini ambayo ni changamoto kubwa kwa wananchi wa mkoa huo.

Alisema japo mkoa huu unatajwa kama makao makuu ya serikali lakini mkoa huu ni wa tatu kutoka mwisho kaytika mikoa maskini zaidi hapa nchini.

“Mkoa wa Dodoma ni wa 19 kati ya mkoa 21 ya Tanzania Bara kiuchumi na wakati ina rasilimali nyingi sana za kiuchumi kama ilivyo kwa mikoa mingine hapa nchini,” alisema Zitto na kuongeza kuwa

“…Dodoma ni mojawapo ya mikoa yenye uchumi duni nchini. Kwa kutumia kigezo cha wastani wa pato la mtu kwa mwaka ya ni moja kati ya mikoa mitano yenye uchumi duni kuliko yote nchini.

Umaskini umekithiri na upo ushahidi wazi kuwa huduma za kimsingi zimeendelea kushuka kadri miaka inavyozidi kwenda, kutokana na viwango vidogo vya bajeti ya Serikali ya CCM,” alisema Zitto.

Amesema Mkoa wa Dodoma pamoja na kuwa mifugo pamoja na kilimo cha zabibu na mahindi lakini bado wananchi wake wamekuwa ni maskini wa kutupwa hali inayosababishwa na viongozi wa Serikali.

“Dodoma haina maji ya uhakika, lakini bado imekuwa ikikubwa na migogoro ya ardhi kati ya wananchi na CDA huku viongozi wake wakibaki kuangalia tu, sisi ACT-Wazalendo hatutaki jambo hili na leo tumewalete achama kipya ambacho kinajenga matumaini mapya kwa Tanzania mpya.

Naye mwenyekiti wa chama hicho Anna Mghwira alisema kuwa chama hicho kitasimamisha mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa mujibu wa ilani ya chama hicho.

Pamoja na hali hiyo kimetangaza mgombea wake atapokea matokea ya urais na kuapishwa katika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa kama njia ya kuenzi misingi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ya kutaka Serikali ihamie Dodoma.

Amesema hivi sasa kila Mtanzania amekuwa akihoji chama hicho iwapo kitasimamisha mgombea urais, alisema ilani ya ACT-Wazando imeweka wazi misingi na wajibu wa kiongozi kwa Taifa ikiwemo kuzingatia miiko ya uongozi ulioasisiwa na Azimio la Arusha.

“Ilani yetu ACT ipo wazi kwa kila Mtanzania na hivi sasa hoja kubwa je tutasimamisha mgombea au laa, jibu ni jepesi kabisa ndio tutasimamisha lakini kwa mujibu wa ilani yetu na atalazimika kusaini miiko na maadili ya uongozi wa chama chetu, kwa hiyo kama mnasikia kuna watu wanatajwa sawa acha watajwe lakini mgombea wetu ili uweze kuwa mwanachama je wataweza miiko na maadili ya chama kwa umma,” alisema Anna.