Wednesday , 28th Jan , 2015

Tukio la polisi kudaiwa kumpiga, kumdhalilisha na kumshikilia mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Prof  Ibrahimu Lipumba na baadhi ya viongozi waandaamizi wa chama hicho, limeingia katika sura mpya.

Tukio hilo limesababisha bunge kushindwa kuendelea na utaratibu wake kwa mujibu ratiba baada ya spika kukataa hoja ya kuahirisha shughuli za bunge ili kujadili suala hilo huku akiitaka serikali kutoa tamko Alhamisi ya January 29 bungeni ili suala hilo lijadiliwe jambo lililogomewa na wabunge wa upinzani.

Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni kwa mujibu wa ratiba shughuli iliyokuwa inafuata ni kuwasilishwa kwa taarifa za kamati za bunge na kisha kujadiliwa.

Kabla ya hatua hiyo akasimama Mh James Mbatia kwa kutumia kanuni ya 47 ya kanuni za bunge kutaka bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili suala la dharura ambalo limedaiwa ni kudhalilishwa na kupigwa na polisi kwa Prof Ibrahim Lipumba kwa kile kilichodaiwa ni amri kutoka juu.
 
Mara baada ya kutolewa hoja hiyo spika Anne Makinda akaitaka serikali kutoa tamko juu ya tukio hilo siku ya Alhamis ya January 29, 2015 na kisha wabunge wajadili suala liligomewa na wabunge wa upinzani kwa mtindo wa kusimama na kupiga kelele badala ya kutoka nje kama ilivyozoeleka.
 
Kufuatia kelele hizo za waheshimiwa wabunge kushinikiza jambo hilo lijadiliwe hii leo spika Anne Makinda akaahirisha shughuli za bunge kwa wakati huo.
 
Nje ya bunge baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani na chama tawala wakatoa maoni yao kuhusu kuahirishwa kwa bunge, ambapo mbunge Ester Bulaya na Mwigulu Nchemba wameshangazwa na hatua ya wabinge wa upinzani kugomea uamuzi wa Spika na kusema kuwa Spika ametumia busara na ujasiri kukubali hoja hiyo ijadiliwe, kwahiyo wabunge walitakiwa kumuunga mkono ili hoja hiyo ijadiliwe kesho badala ya leo.
 
Wabunge wa upinzani mara baada ya kutoka nje wakajifungia katika ukumbi wa Pius Msekwa hata hivyo haikufahamika mara moja suala walilokwenda kulijadili.

Wakati wa jioni, ambapo bunge lilikuwa liendelee, Spika Makinda alilazimika kuliahirisha tena kwa madai kuwa wamekuwa na majadiliano ya muda mrefu kuhusu hoja ya Mbatia, na wamekubaliana kwamba kikao hicho kisiendelee hadi kesho (Alhamis 29, February) saa 3.00 Asubuhi.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook mwenyekiti wa kamati ya Hesabu za serikali Zitto Kabwe amesema kuwa hayuko tayari kuendelea na taarifa yake ikiwa kuna mambo yanayokiuka haki za binadamu yameachwa bila kujadiliwa.

Zitto amesema
"Kwanini sikwenda kusoma taarifa ya PAC leo nilipoitwa na Spika? Jibu rahisi kabisa, siwezi kuona madhila na uvunjifu mkubwa wa HAKI za binaadamu nikaendelea na mambo kama hakuna lililotokea. Kitendo cha polisi kutumia nguvu, kupiga raia hovyo na kumdhalilisha Kiongozi wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba ni kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote."