RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Dk. Shein ambaye alikuwa akizungumza na wananchi wa Wete waliokwenda kumsalimia mara baada ya kukagua ujenzi wa soko na Ofisi ya Baraza la Mji Wete alisema kuwa suala la amani halina mbadala huku akiahidi kuendelea kuisimamia amani ya Zanzibar na kusikitishwa na wale wote wanaotaka kuvuruga amani kwa kisingizio cha kuiongoza Zanzibar.
Alisema kuwa amani na utulivu uliopo ndio msingi wa maendeleo ya Zanzibar hivyo Wazanzibari wanapaswa kuienzi na kuilinda kwa nguvu zao zote.
Dk. Shein alisisitiza kuwa kila mwananchi anataka kuishi kwa amani na utulivu na kuwataka wananchi wa Zanzibar kutambua kuwa wao ni ndugu na kuwasihi baadhi ya wananchi wanaotaka kuvuruga amani na kuendelea kutisha wenzao kwani Zanzibar inaongozwa kwa Sheria na Katiba.
“watu wasihemkwe wala wasichagawe kwani kila mmoja anataka kuishi kwa amani na utulivu sisi ni wamoja wa kusini Pemba, Kaskazini Pemba wa Kusini Unguja na Kaskazini Unguja...tumetofautiana kwa kuishi na kutafuta maisha tu”,alisema Dk. Shein.
Kwa upande wa mradi huo Dk. Shein alirejea kauli yake kama aliyoizungumza wakati akiitembelea miradi kama hiyo katika miji ya Wete na Chake kwa kusema kuwa hizo ni miongoni mwa ahadi zake alizowaahidi wananchi za kuimarisha miji yote ya Zanzibar.